Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema halikumkamata mtu yeyote katika tukio lililotokea eneo la Kariakoo, bali lilichukua hatua ya kuzuia fujo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutokuwepo kwa uwanja rasmi wa kufanyia mkutano wa hadhara katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya habari ya kituo cha runinga cha ITV usiku huu, April 22,2025, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Muliro Jumanne Muliro, amesema watu waliokuwepo katika eneo hilo waliondolewa kwa ajili ya kudhibiti hali ya fujo na msongamano wa watu waliokuwa wakifanya shughuli za biashara, na kwamba hakuna aliyekamatwa wala kushikiliwa.
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, amekamatwa na polisi wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo hilo la Kariakoo.
Mapema kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya kuzuia mkutano wa hadhara wa CHADEMA kufanyika katika eneo hilo, likieleza kuwa eneo la Kariakoo lina msongamano mkubwa wa watu wanaofanya shughuli za kibiashara na mkutano huo ungeweza kuathiri utulivu wa eneo hilo. Polisi walishauri mkutano kufanyika katika maeneo mengine ya wazi yenye nafasi.
Hata hivyo, kupitia taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa X (zamani Twitter), Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Godbless Lema, alieleza kuwa chama hicho kilikwisha kuwasilisha taarifa ya mkutano kwa polisi wiki moja kabla ya tukio, na maandalizi ya mkutano huo yalikuwa yameanza kutangazwa mapema.
Leave a Reply
View Comments