Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi

Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi
Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi
Image with Link Description of Image

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametaka uchunguzi juu ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania, huku ripoti zikiibuka kwamba miili inachukuliwa na vikosi vya usalama na kupelekwa katika maeneo ambayo hayajajulikana.

Taarifa zilizopatikana na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo tofauti nchini Tanzania zinaonyesha mamia ya waandamanaji na watu wengine waliuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa au kushikiliwa. Ofisi imeshindwa kuthibitisha kwa uhuru takwimu za majeruhi kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa intaneti wakati wa kupiga kura.

“Taarifa za familia zinazosaka wapendwa wao kila mahali kwa kutembelea kituo kimoja cha polisi baada ya kingine na hospitali moja baada ya nyingine ni za kutisha. Naomba sana serikali ya Tanzania itoe taarifa kuhusu hatma na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa wapendwa wao ili wazikwe kwa heshima,” amesema Türk.

Image with Link Description of Image

“Pia kuna ripoti kwamba vikosi vya usalama vimeonekana vikiondoa miili kutoka mitaani na hospitalini na kuipeleka kwenye maeneo ambayo hayajajulikana katika jaribio la kuficha ushahidi.”

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu ameitaka Tanzania kuchunguza madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, kikamilifu na kwa uwazi, na kuwawajibisha wale waliohusika.

Ametoa wito kwa mara nyingine kuachiwa huru bila masharti vigogo wote wa upinzani waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu akiwemo kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema Tundu Lissu na watu wengine wote waliowekwa kizuizini tangu siku ya uchaguzi.

Inaarifiwa kuwa zaidi ya watu 150 wametiwa mbaroni tangu siku ya kupiga kura – wakiwemo watoto walioshtakiwa kwa uhaini.

“Ni muhimu wale wote waliokamatwa au kuzuiliwa kwa makosa ya jinai wawasilishwe mara moja mbele ya a mahakama. Na wale wote wanaozuiliwa lazima wapewe haki kamili chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Türk.