Wanafunzi 17 wafariki baada ya moto kuteketeza bweni Kenya
Wanafunzi 17 wa shule ya msingi ya Hillside Endarasha wamefariki baada ya bweni lao kuungua moto usiku wa kuamkia leo. Wanafunzi hao wameteketezwa kiasi cha kutotambulika huku wengine 13 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Rais William Ruto ameagiza uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto.
Msemaji wa Idara ya polisi ya Kenya Resilia Onyango amesema moto huo ulizuka kwenye bweni moja ambalo lilikuwa na wanafunzi 152 wa kiume. Shughuli ya uokoaji ingali inaendelea kwenye shule hiyo ya msingi ya Hillside Endarasha huko kaunti ya Nyeri, eneo la kati ya Kenya, takriban kilomita 153 Kaskazini mwa mji mkuu Nairobi.
Wazazi wameanza kufika shuleni hapo na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu wameweka dawati la kutoa huduma za ushauri nasaha kwa familia zilizoathirika, huku wakiwasaidia wazazi kuwatafuta na kuwatambua watoto wao.
Msimamizi wa shirika la msalaba mwekundu eneo la kati, Esther Chege, amefika kwenye eneo la mkasa pamoja na timu ya wataalamu wengine.
“Tumekuja hapa kuungana nanyi na kuungana na serikali kuhakikisha kwamba tumeweza kusaidiana. Tunatoa huduma ya ushauri nasaha siku ya leo na tutaendelea hadi oparesheni hii itakapokamilika. Tunawalenga watoto, wazazi na jamii nzima. Tunawashukuru wanajamii kwa kujitokeza haraka sana kutoa usaidizi.”
Viongozi mbalimbali wametoa risala za rambirambi kufuatia mkasa huo wa moto shuleni. Rais William Ruto ametuma rambirambi kwa familia zilizoathirika akikitaja kisa hicho kama cha kuvunja moyo. Amewaagiza maafisa wa usalama kuchunguza kisa hicho na kuhakikisha kuwa wahusika wamechukuliwa hatua.
Rais Ruto ameahidi kuwa wizara ya usalama inafanya kila juhudi kuzisaidia familia zilizoathirika. Naibu rais Rigathi Gachagua, Kiongozi wa chama cha upinzani ODM Raila Odinga, spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, na mawaziri wengine pia wametuma ujumbe wa kuzifariji familia zilizoathirika.
Gavana Mutaji Kahiga pia amefika kwenye eneo la mkasa na kuelezea masikitiko yake.
“Hili ni jambo ambalo limetugonga sana, tumejaribu tuwezavyo, kama mnavyojua magari yalijaribu kufika hapa na tatizo la barabara pengine lilitatiza na hayakuweza kufika kwa haraka kama tulivyokusudia. Ni kizazi ambacho tulikuwa na matarajio mengi nacho, nampa pole pia mwalimu mmiliki wa shule, tulikuwa hapa juzi na tukazungumza na Watoto, ni shule ambayo ilikuwa inafanya viruzi.”
Chanzo cha moto wenyewe hakijabainika ingawaje baadhi ya maafisa wanaeleza kwamba majengo mengi ya eneo hilo yamejengwa kwa mbao na sio saruji, na bweni hilo pia lilikuwa limejengwa kwa mbao, na huenda moto huo ulitembea kwa kasi zaidi kutokana na mbao hizo.