Wanajihadi wanadai kuchukua madaraka nchini Syria
Wanajihadi na wanamgambo wengine wanaoipinga serikali waliingia Damascus siku ya Jumamosi, wakichukua udhibiti wa mji huo mkuu wa Syria. Wametangaza jiji hilo kuwa “huru” kutoka kwa serikali ya Rais Bashar Assad na kudai kwamba ameukimbia mji mkuu.
Kulingana na Reuters, Assad, ambaye alitawala nchi hiyo ya Mashariki ya Kati kwa karibu robo karne, alikimbia kutoka Damascus siku ya Jumamosi jioni “kwenda kusikojulikana,” likinukuu taarifa za maafisa wawili wakuu wa jeshi. Saa kadhaa kabla ya hapo, wanajihadi hao walitangaza kwamba walikuwa wameudhibiti kikamilifu mji muhimu wa Homs baada ya siku moja tu ya mapigano.
Waziri Mkuu nchi hiyo Mohammad al-Jalali ametoa ushirikiano “na uongozi wowote uliochaguliwa na watu,” akiongeza kuwa bado yuko nyumbani kwake.
HTS, kundi linaloongozwa na kamanda wa zamani wa Al-Qaeda na hapo awali likiijulikana kama Jabhat al-Nusra, lilianzisha mashambulizi ya kushtukiza kutoka mkoa unaoshikiliwa na upinzani wa Idlib kaskazini mwa Syria wiki iliyopita. Wanajihadi tayari wameliondoa Jeshi la Syria kutoka miji ya Aleppo, Hama, Homs, na Al-Qusayr kwenye mpaka na Lebanon.
Jeshi Huru la Syria (FSA) linaloungwa mkono na Marekani limechukua udhibiti wa eneo la kale la Palmyra, huku Jeshi la Syrian Democratic Forces (SDF) kinaloungwa mkono na Marekani pia likiiteka eneo la Deir ez-Zor mashariki mwa nchi hiyo.
Mamlaka ya Syria imejiingiza katika migogoro kadhaa ya kienyeji tangu mwaka 2011, wakati makundi mbalimbali yanayoipinga serikali yalipojaribu kwanza kumng’oa Assad. Vikosi vya kijihadi, haswa vile vinavyopokea usaidizi wa kijeshi kutoka nje ya nchi, vimeibuka kuwa wachezaji wakuu kati ya upinzani.