Yanga Yafunga mwaka 2024 kibabe ikiifumua Fountain 5-0

0
Yanga Yafunga mwaka 2024 kibabe ikiifumua Fountain 5-0

YANGA ni kama imejibu mapigo kwa watani wao wa Simba, baada ya jioni hii kupata ushindi wa kishindo wa mabao 5-0 dhidi ya Fountain Gate ambayo mara baada ya mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam ilitangaza kulivunja benchi lote la ufundi chini ya kocha Mohammed Muya.

Ushindi huo wa leo umeifanya Yanga kuibana Simba kileleni kwa kutofautiana pointi moja tu baada ya kila moja kucheza mechi 15 za duru la kwanza baada ya jana kushinda bao 1-0 ugenini na kuifanya ifikishe pointi 40, wakati watetezi hao wamefikisha 39 na zote kulingana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ushindi huo wa 5G ni wa kwanza kwa Yanga msimu huu, lakini ni wa tano mfululizo kwa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara tangu iwe chini ya kocha Sead Ramovic aliyempokea Miguel Gamondi aliyefurushwa baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo za Azam (1-0) na Tabora United iliyoshinda 3-1 zote ikiwa nyumbani.

Pia ushindi huo umeufanya Yanga ya Ramovic kukusanya jumla ya mabao 18-2, kwani ilianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo ugenini, kisha ikazitambia Mashujaa (3-2), Tanzania Prisons 4-0 na huu wa leo dhidi ya Fountain (5-0), mbali na 4-0 iliyopata ugenini dhidi ya Dodoma Jiji katikati ya wiki hii.

Mabao hayo yameifanya Yanga katika mechi 15 iwe imefunga jumla ya mabao 32 na kufungwa sita, huku Simba ikifunga 31 na kuruhusu matano na kuzifanya zote kuwa na tofauti na 26 kupuitia mechi hizo.

Ushindi wa Yanga ulitengenezwa mapema katika dakika 45 za kwanza, baada ya kufunga mabao matatu yaliyowekwa na Pacome Zouzoua dakika ya 16 na 45’+1 akimalizia pasi tamu za Chadrcak Boka na Clement Mzize, kabla ya Mzize kumtengenezea tena Mudathir Yahya dakika ya 41. Hilo lilikuwa bao la kwanza kwa muda katika Ligi Kuu msimu huu, lakini ikiwa ni asisti ya tatu kwa Mzize hadi sasa.

Mabao hayo yaliizima Fountain ambayo ilimaliza dakika 45 za kwanza ikipiga shuti moja tu lililolenga lango huku Yanga ikitaka zaidi kipindi hicho ikishambulia kwa haraka na kutengeneza uongozi huo na kama sio umakini mdogo wa Pacome, Prince Dube, Mzize na Stephane Aziz KI bado karamu ingekuwa kubwa zaidi.

Katika dakika 45 hizo za kwanza beki mpya wa Fountain, Mtenje Albano aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Dodoma Jiji, alijikuta akifungwa mdomo baada ya awali kutamba kabla ya mchezo kwamba hajawahi kupoteza mchezo mbele ya Yanga kwa mastaa wa Jangwani kuimjibu kwa vitendo.

Beki huyo aliruhusu bao la kwanza lililotokana na krosi ya Boka aliyekuwa upnade anaocheza na kumfikia Pacome aliyefunga kiulaini kwa kichwa, kisha timu zilipoenda mapumziko hakurudi uwanjani baadaya nafasi yake kuchukuliwa na beki mwingine mpya kutoka Coastal Union, Jackson Shiga.

Shiga naye aliiosaidia Yanga kuongeza idadi ya mabao baada ya kujifunga bao la nne wakati alipogongwa na mpira wa shuti la Pacome lililoparazwa na kipa John Noble na kugonga mlingoni wa lango naye kuusindikiza wavuni akiwa mbele ya Dube aliyekuwa akivizia kufunga, hiyo ikiwa ni dakika ya 52.

Wakati Fountain wakijiuliza watayarudisha vipi mabao hayo, Mzize alifunga chuma cha tano dakika ya 88 akimalizia pasi ndefu ya mtokea benchi, Salum Abubakar na kuuchopu mpira mbele ya kipa Noble aliyekuwa ametoka kukabiliana naye na kuishia kusindikizwa na beki wa kati na nahodha wake, Laurian Makame.

Hilo lilikuwa bao la sita kwa Mzize msimu huu na kumfanya awe kinara kwa wachezaji wa Yanga, akiwaacha nyuma Pacome na Dube ambao kila mmoja akiwa na matano, huku beki Ibrahim Bacca akiwa na manne.

KMC, COASTAL NGOMA DROO

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa muda mmoja na ile ya Yanga na Fountain, ikipigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha wenyeji Coastal Union ililazimika kuchomoa bao ‘jioni’ na kutoka sare ya 1-1 na KMC iliyotangulia kwa bao la mapema dakika ya kwanza kupitia kwa Deogratius Kulwa.

Coastal ilipata penalti dakika ya 90’+1′ lililowekwa wavuni na Maabad Maulid, japo marudio ya Azam TV haikuonyesha mchezaji aliyenawa mpira kama ilivyotafsiriwa na mwamuzi wa mchezo huo.

Source: Mwanaspoti

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *