Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amewasili mkoani Iringa kutoa pole kwa familia ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Mkoa wa Iringa, Ibrahimu Myovela, pamoja na familia za wenzake wawili Antony Mwasika na Ally Kalolo, ambao wanadaiwa kupotea wakiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi mkoani humo.
Heche alifika nyumbani kwa wazazi wa Ibrahimu Myovela na kutoa salamu za pole kwa niaba ya chama hicho, huku akiihakikishia familia kuwa CHADEMA itaendelea kusimama pamoja nao katika kuhakikisha vijana hao wanapatikana na kurejeshwa salama kwa familia zao.
Katika mazungumzo yake, Heche aliwataka Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kuwatafuta vijana hao na kutoa taarifa sahihi kwa umma, akisisitiza kuwa mazingira ya kutoweka kwao yanadaiwa kuhusishwa na jeshi la polisi baada ya kushikiliwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Februari 10, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, vijana hao wanatuhumiwa kuhusika katika tukio la kujeruhi lililosababisha kifo . Taarifa hiyo ya polisi inaeleza kuwa baada ya tukio hilo, Ibrahimu Myovela na wenzake walidaiwa kutoroka huku jeshi la polisi likisema linaendelea kuwatafuta kwa tuhuma za mauaji.




Leave a Reply
View Comments