Israel yashambulia maeneo 40 ya urushaji makombora Lebanon

0
Israel yashambulia maeneo 40 ya urushaji makombora Lebanon

Israel yashambulia maeneo 40 ya urushaji makombora Lebanon

Hezbollah ilisema ilifyatua maroketi 320 chapa ya Katyusa kuelekea Israel na kupiga shabaha 11 za kijeshi katika kile ilichokiita awamu ya kwanza ya kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya Fuad Shukur, kamanda wa juu wa Hezbollah, mwezi Julai.

Jeshi la Israel lilisema lilizuwia shambulio kubwa zaidi kwa mashambulizi ya kuzuwia, baada ya kutathmini kwamba Hezbollah ilikuwa inajiandaa kufanya mashambulizi makubwa, kwa kutumia ndege 100 kushambulia zaidi ya vituo 40 vya ufyatuaji vya Hezbollah kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi hayo yaliharibu mamia ya mifumo ya maroketi yalioelekezwa hasa kaskazini mwa Israel lakini pia yalilenga shabaha katika baadhi ya maeneo ya katikati mwa Israel, lilisema jeshi la Israel.

Hezbollah ilitupilia mbali taarifa ya Israel kwamba mashambulizi ya kundi hilo yamezimwa na mashambulizi ya kuzuwia, ikisema kuwa imeweza kurusha droni zake kama ilivyopangwa na kwamba majibu yake mengine kwa mauaji ya Shukr yatachukua “muda”.

Baraza la mawaziri la Israel lilikutana majira ya moja asubuhi. Waziri wa ulinzi Yoav Gallant alitangaza hali ya dharura na waziri wa mambo ya nje Israel Katz alisema Israel itajibu matukio yanayondelea lakini hakutaka vita kamili.

Safari za ndege kwenda na kutoka uwanja wa Ben Gurion mjini Tel Aviv zilisitishwa kwa karibu dakika 90.

“Tumedhamiri kufanya kila kitu kinachowezekana kulinda nchi yetu, kuwarejesha salaama wakazi upande wa kaskazini majumbani mwao na kuendelea kushikilia kanuni rahisi: Yeyote anaetudhuru – tunamdhuru,” alisema waziri mkuu Benjamin Netanyahu katika taarifa.

Waziri Mkuu wa muda wa Lebanon Najib Mikati alikutana na mawaziri katika kikao cha kamati ya taifa ya dharurua. Kiongozi wa Hezbollah alitarajiwa kuzungumza kupitia televisheni baadae Jumapili, lilisema kundi hilo.

Ikulu ya Marekani, White House, ilisema Rais Joe Biden alikuwa anafuatilia matukio hayo kwa karibu.

“Kwa maelekezo yake, maafisa wakuu wa Marekani wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara na wenzao wa Israel. Tutaendelea kuunga mkono haki ya Israel kujilinda, na tutaendelea kufanyia kazi utulivu wa kikanda,” alisema msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa Sean Savett.

Hezbollah ilirusha makombora dhidi ya Israel mara tu baada mashambulizi ya Oktoba 7 yaliofanywa na wapiganaji wa Hamas dhidi ya Israel. Hezbollah na Israel zimekuwa zikishambuliana mara kwa mara tangu wakati huo, huku zikiepusha ongezeko kubwa wakati vita vikiendelea Gaza.

Mizani hiyo ya hatari ilionekana kubadilika baada ya mashambulizi kwenye Milima ya Golan, ambayo Hezbollah ilikanusha kuhusika nayo, na mauaji yaliyofuatia ya Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa kijeshi wa Hezbollah.

Kifo cha Shukr katika shambulio la anga kilifuatiwa haraka na mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran, ambayo yalisababisha viapo kutoka Iran, vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *