Kiongozi wa mrengo wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, ameuawa pamoja na mmoja wa walinzi wake mjini Tehran, kundi la Palestina na mamlaka za Iran zimethibitisha.
Hamas iliharakisha kulaumu mauaji hayo kwa Israel, ambayo hadi sasa imekataa kuzungumzia lolote.
Kundi hilo limesema Haniyeh aliuawa Jumanne asubuhi katika “shambulio la kihaini la Wazayuni kwenye makazi yake” huko Tehran.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) limesema uchunguzi unaendelea.
Haniyeh, ambaye kwa kawaida anaishi Qatar, alikuwa katika mji mkuu wa Iran kwa ajili ya kuapishwa kwa rais mpya, Masoud Pezeshkian.
Mauaji ya Haniyeh ni “kitendo cha uoga ambacho hakitapita bila kuadhibiwa”, kituo cha televisheni cha Hamas cha Al-Aqsa kilimnukuu afisa mkuu wa Hamas Moussa Abu Marzouk akisema.
“Mauaji haya yaliyofanywa na Israel kwa Ndugu Haniyeh ni ongezeko kubwa ambalo linalenga kuvunja dhamira ya Hamas,” afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri aliiambia Reuters. Aliendelea kusema kwamba Hamas itaendeleza njia inayofuata, na “ina uhakika wa ushindi.”
Israel ilikuwa imetishia kumuondoa Haniyeh na viongozi wengine wa Hamas juu ya shambulio la Oktoba 7 la kundi hilo dhidi ya Israel ambalo liliua watu 1,200 na kuona wengine 250 wakichukuliwa mateka. Mapema mwaka huu mashambulizi ya anga ya Israel katikati mwa Gaza yaliwaua watoto watatu wa kiume na wajukuu wanne wa Haniyeh. Wanajeshi walidai walihusika katika “shughuli za kigaidi”. Haniyeh wakati huo alisema kuwa takriban watu 60 wa familia yake waliuawa tangu Oktoba.
Kutoka Qatar, Haniyeh alikuwa kiongozi wa wanadiplomasia wa kundi hilo la wanamgambo, akifanya kama mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na mazungumzo ya kurejea kwa mateka wa Israel wakati wa vita vya Israel-Hamas.
Leave a Reply