Baada ya upande wa jamhuri kukiri kuendelea na shauri, Lissu anasimama na kusema.
Lissu: Waheshimiwa majaji mnamo tarehe 8 Septemba mwaka jana 2025 ,niliambiwa na mahakama hii kwamba kesi hii itaamua kama kwa sheria za nchi hii inawezekana kwa kiongozi wa kisiasa au kwa mtu mwingine yoyote kuhumumiwa kifo kwa kuzungumza maneno ya kisiasa kwenye mkutano wa kisiasa, waheshimiwa majaji leo takribani mwaka mmoja baadaye, nimesimama mbele yenu majaji kuwaambia kwamba kwa sheria za Tanzania na kwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapa jambo hilo haliwezekani.
Ninaomba nirudie nimesimama mbele yenu majaji kuwaambia kwamba kwa sheria za Tanzania na kwa ushahidi uliotolewa mahakamani niko hapa kuwaonesha kwamba hilo jambo haliwezekani.
Nilikamatwa katika mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma jioni ya siku ya tarehe 9 April ya mwaka jana 2025, na nilikamatwa nikizungumza kwenye mkutano halali wa hadhara wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA, Chama ambacho nimekiongoza tangu tarehe 22 January 2025… baada ya kukamatwa huko nilisafirishwa usiku huo huo hadi hapa Dar es salaam ambapo waheshimiwa majaji mchana wa kesho yake 10, April 2025 nilisomewa mashtaka kwenye kesi mbili zilizofunguliwa dhidi yangu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Lissu:Waheshimwa majaji katika kesi ya kwanza nilisomewa shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu 82 b, katika kesi ya pili nilisomewa shtaka la kutoa taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 16 ya sheria ya makosa ya mtandao, kesi ambayo imenileta mbele yenu leo.
Hii inatokana na kesi ya kwanza niliyosomewa mahakama ya Kisutu yaani Uhaini, baada ya takribani miezi 4 na nusu ya mashauri katika mahamaka ya hakimu mkazi Kisutu, Mkurugenzi wa Mashtaka DDP aliwasilisha taarifa kwenye mahakama hii kuhusiana na hilo shtaka la uhaini, taarifa yenyewe ni ya tarehe 12, Agosti 2025.
Taarifa hii inanituhumu kwa mambo yafuatayo;
Kwamba nikiwa chini ya utiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nilitengeneza nia ya kuhamasisha Umma kuwezesha kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 kwa lengo la kuitishia serikali ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, na nilidhihirisha nia hiyo kwa kitendo changu cha kutamka au kusema na kuchapisha maneno yafuatayo;
“Wanasema kitu kimoja sahihi hapa wanasema hivi msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hii ndiyo namna ya kupata mabadiliko kwa hiyo tunaenda kukinukisha sana sana huu uchaguzi tutauvuruga, tutauvuruga huu uchaguzi kwa sababu tunaenda kukinukisha vibaya sana.”





Leave a Reply
View Comments