Majina ya waliopata mkopo awamu ya kwanza 2024/2025
Majina ya waliopata mkopo awamu ya kwanza 2024/2025
Ni awamu ya kwanza yenye wanafunzi 21,509
Mikopo yao ina thamani ya TZS 70.78 bilioni
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo Jumamosi (Septemba 28, 2024) imeanza kutangaza orodha ya wanafunzi wenye sifa waliopangiwa mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2024/2025. Awamu hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ya Shahada ya awali, Shule ya Sheria kwa Vitendo na Shahada ya Uzamili.
Wanafunzi kupata taarifa kupitia SIPA
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia amesema wanafunzi wote walioomba mikopo kwa mwaka 2024/2025 wanaweza kupata taarifa za kina kuhusu mikopo yao kupitia akaunti walizotumia kuombea mikopo maarufu kama‘SIPA’ – Student’s Individual Permanent Account.
“Leo tumeanza kutoa taarifa za mikopo kwa makundi yote, waliopangiwa mikopo, wapo ambao bado tunaendelea kufanyia kazi maombi yao … kila mwombaji anapata taarifa yake kwenye akaunti ile ile aliyotumia kuombea mkopo, huhitaji kufika ofisi za HESLB”, amesema Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada ya Uzamivu unaendelea.
Dkt. Kiwia amesema HESLB imeanza kuandaa malipo ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo ambao ni wanufaika wa mikopo na kusema lengo ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kwa wakati.
245,799 kunufaika na mikopo 2024/2025
“Mwaka huu, Serikali imetenga TZS 787 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 245,799 wakiwemo zaidi ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza waliotengewa TZS 284.8 bilioni,’ amesema Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa bajeti ya mwaka 2024/2025 imeongezeka kwa TZS 38 bilioni sawa na asilimia 5.1 ikilinganishwa na bajeti ya 2023/2024 iliyokuwa TZS 749.4 bilioni. Mwaka huu pia kiwango cha chini cha mkopo kwa mnufaika mmoja mmoja kimepanda hadi TZS 3.0 milioni kutoka TZS 2.7 milioni[ME1] mwaka uliopita wa2023/2024.
Wito: Vyuo kuwasilisha matokeo ya mitihani
Kuhusu wajibu wa vyuo, Dkt. Kiwia amevikumbusha vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi-wanufaika wanaoendelea na masomo, kuwasilisha ili kuiwezesha HESLB kuandaa malipo kwa wakati.
“Kuna vyuo vichache, ambavyo bado havijawasilisha matokeo, tumewakumbusha na tunasisitiza waharakishe kuwasilisha matokeo ili tukamilishe malipo ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na masomo,” amesema Dkt. Kiwia.
Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Pili
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB amesema kuwa awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi waliopangiwa mikopo kwa mwaka 2024/2025 itatangazwa wiki ijayo.