Marekani na Israel zaonya kuhusu athari mbaya baada ya shambulio la makombora la Iran
Marekani na Israel zinasema zinafanya kazi pamoja ili kuhakikisha Iran inakabiliwa na mashambulizi makali ya kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya makombora takribani 200 hivi ya masafa marefu dhidi ya Israel usiku wa Jumanne.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa ya video kwa lugha ya Kiebrania, kwamba “Iran ilifanya makosa makubwa, na Israell italipa,” akisema kwamba mashambulio hayo dhidi ya taifa la Kiyahudi la Israel yameshindwa pakubwa.
“Utawala wa Iran hauelewi azma yetu ya kujilinda na azma yetu ya kulipiza kisasi dhidi ya maadui zetu … Wataelewa. Tutasimama kwa kanuni tuliyoweka: Yeyote atakayetushambulia, tutawashambulia.”
Mapema siku hiyo, ving’ora vya mashambulizi ya anga vilisikika kote kwa urefu na upana wa Israel muda mfupi baada ya Marekani kutangaza kuifahamisha Israel juu ya dalili kwamba Iran iko tayari kufanya shambulio hilo mara moja.
Israel ilifunga kwa muda anga yake kwa kwa kutumia mifumo ya ulinzi wa makombora ikimulika angani usiku juu ya Tel Aviv na Jerusalem, lakini baadhi ya picha nyingine ambazo hazijathibitishwa kutoka kwenye mitandao ya kijamii zilionekana kuonyesha makombora yakianguka ardhini nchini Israel.
Marekani ilisema inafanya kazi na Israel katika kujibu mashambulizi ayo.
“Tutashauriana na Waisraeli juu ya hatua zinazofuata katika suala la majibu”, Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani Jake Sullivan alisema, akisema kwamba meli za majini za Marekani zilisaidia kukabiliana na makombora yaliyokua yanaelekea Isreal.
“Tumeweka wazi kuwa kutakuwa na matokeo, madhara makubwa kwa shambulio hili, na tutashirikiana na Israel kufanya hivyo,” akiongeza kuwa shambulio hilo “limeshindwa na halikufanyi kazi”.
Jeshi la Israel limetaja idadi ya makombora ya Iran yaliyoingia kuwa karibu 200.
Taarifa za habari za ndani zilionyesha kuwa Mpalestina mmoja katika eneo la Jeriko katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel aliuawa baada ya jeshi la Israel kusema kuwa halina dalili za mara moja za majeraha au vifo.
Makamu wa Rais wa Marekani na mgombea wa kiti cha Rais wa chama cha Democratic aliionya Iran au washirika wake wenye silaha dhidi ya kushambulia vikosi vya Marekani katika eneo hilo.
“Siku zote nitahakikisha Israel ina uwezo wa kujilinda dhidi ya Iran na wanamgambo wa kigaidi wanaoungwa mkono na Iran,” Harris aliwaambia waandishi wa habari. “Kamwe hatutasita kuchukua hatua zozote zinazohitajika kutetea vikosi na maslahi ya Marekani dhidi ya Iran na magaidi wanaoungwa mkono na Iran”. Kamala alisema
Iran ilieleza shambulio hilo kama jibu halali kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya raia na maslahi yake.
“Majibu ya kisheria, ya kimantiki na ya kihalali ya Iran kwa vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni – ambavyo vilihusisha kuwalenga raia na maslahi ya Iran na kukiuka mamlaka ya kitaifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran – yametekelezwa ipasavyo,” ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa, ulisema katika chapisho kwenye mtandao wa X.
SOMA PIA: Israeli ilishambuliwa kwa makombora ya hypersonic ya Iran
“Iwapo utawala wa Kizayuni utathubutu kujibu au kufanya vitendo vya udhalimu zaidi, majibu ya baadaye na ya kutisha yatatokea. Mataifa ya kikanda na wafuasi wa Wazayuni wanashauriwa kuachana na utawala huo.” Irani ilisema
Katika kuelekea mashambulizi hayo, Kamandi Kuu ya Marekani, kikundi cha kijeshi kinachohusika na Mashariki ya Kati, kilitangaza kuwa vikosi vitatu zaidi vya ndege vikiwemo F-15, F-16, na ndege za kivita za A-10 vinawasili katika eneo hilo na kwamba kikosi kimoja tayari kimefika.
Bei ya mafuta ilipanda karibu dola 6 kutoka bei ya juu ya $72 kwa pipa katika ishara ya hofu kuhusu njia kuu ya usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango wa Hormuz unaozunguka Iran.
Israel ilizindua kile ilichokiita uvamizi mdogo wa ardhini ndani ya Lebanon siku ya Jumatatu ambayo ilisema inalenga kuwaondoa Hezbollah kutoka vijiji vya mpakani vinavyorusha makombora katika jamii za Kaskazini mwa Israel.
Israel kwa muda wa wiki mbili imekuwa ikikabiliana na wanamgambo wa kundi Hezbollah waoungwa mkono na Iran nchini Lebanon, na kumuua kiongozi wa kundi hilo Hassan Nasrallah katika shambulio la angani la Beirut siku ya Ijumaa.
SOMA ZAIDI: Hezbollah wapo ‘tayari’ kwa operesheni ya ardhini ya Israeli – naibu kiongozi wa Hezbolaah
Mashambulizi hayo yamewauwa hadi watu 1,000 nchini lebanon wakiwemo raia wengi lakini pia viongozi wakuu wa Hezbollah na wapiganaji wa kundi hilo.
Kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh aliuawa katika mlipuko Tehran mwezi Julai katika mauaji ambayo yanalaumiwa kufanywa na Israel.
Iran mwezi Aprili ilirusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya Israel katika shambulio lake la kwanza la moja kwa moja katika eneo la Israel kulipiza kisasi shambulio la anga la Israel dhidi ya ubalozi wa Iran mjini Damascus.
Marekani, pamoja na madola ya Magharibi na baadhi ya mataifa ya Kiarabu yaliisaidia Israel kujikinga na mashambulio hayo.
Iran na washirika wake wenye silaha katika eneo lote wamekuwa wakikabiliana na Israel tangu wanamgambo wa Hamas wa Palestina walipoishambulia Israel tarehe 7 Oktoba.