Rais wa Malawi aagiza wanajeshi wake kujiandaa kuondoka Mashariki mwa DRC

Rais wa Malawi aagiza wanajeshi wake kujiandaa kuondoka Mashariki mwa DRC

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amemuagiza kamanda wa jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoa majeshi ya Malawi kutoka eneo la Mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kulingana na taarifa Televisheni ya serikali.

Taarifa hiyo ilisema uamuzi wa rais unalenga “kuheshimu tangazo la kusitisha mapigano kati ya pande zinazozana,” ingawa uamuzi wa kusitisha mapigano ulikuwa ni mpango wa waasi wa M23 ambao ulitibuka baada ya kundi hilo kushambulia Nyabibwe katika Jimbo la Kivu Kusini mwa DRC.

Image with Link Description of Image

Kuondolewa kwa wanajeshi wa Malawi “kutatoa nafasi mazungumzo yaliyopangwa kuelekea amani ya kudumu,” iliongeza taarifa hiyo.

Rais Lazarus Chakwera amekuwa chini ya shinikizo la kuondoa majeshi ya nchi yake Mashariki mwa DRC baada ya wanajeshi watatu wa Malawi kuuawa katika mashambulizi ya M23 mjini Goma.

Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Kusini mwa Afrika uliotumwa na SADC kusaidia mamlaka ya Congo kukabiliana na makundi yenye silaha katika eneo la mashariki linalokabiliwa na mzozo.

Kufuatia M23 kuuteka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, wamekuwa wakitafuta kuteka maeneo ya Kivu Kusini, hasa mji mkuu Bukavu. Kundi hilo limeteua maafisa wakuu akiwemo gavana wa Kivu Kaskazini, kusimamia eneo hilo.

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 3000 waliuawa wakati wa makabiliano makali ya M23 ya kuiteka Goma.

Kuna hofu kwamba magonjwa kama Mpox na kipindupindu yanaweza kuenea nje ya jiji.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top